WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema kuanzia Machi mosi, 2017 Serikali itapiga
marufuku matumizi ya pakiti za plastiki kufungashiwa pombe kali maarufu
kwa jina la ‘viroba’.
“Tumekaa
na wenye viwanda na kukubaliana kuwa wanaotengeneza Pombe waziweke
katika ukubwa unaokubalika. “Sasa hivi viroba vimeenea kila kona hata
watoto wa shule za msingi wanatumia kwa sababu ni rahisi kuweka mfukoni
na kutembea navyo. Kuanzia tarehe moja Machi, tutakayemkamata ameshika
pombe ya viroba, sisi na yeye.”
Ametoa
kauli hiyo jana jioni (Alhamisi, Februari 16, 2017) wakati akizumgumza
na maelfu ya wakazi wa mji mdogo wa Mererani, wilayani Simanjiro akiwa
katika siku ya pili ya ziara yake mkoani Manyara.
Amesema
agizo hilo linaenda sambamba na vita dhidi ya dawa za kulevya kwani mji
wa Mererani unaongoza kwa matumizi ya dawa hizo haramu.
“Tutawakamata
wanaosambaza, wanaouza na wanaokula. Hapa Mererani kuna bangi, kuna
mirungi, cocaine na heroine. Mkuu wa Mkoa hapa panahitaji operesheni
kupambana na dawa za kulevya. Piteni kwenye vijiwe na kukagua wale
waliolegealegea, kisha tuwapime,” alisisitiza.
Akifafanua
suala la uwekezaji kwenye eneo la Shambalai kutokana na ujumbe
ulioandikwa kwenye mabango, Waziri Mkuu alisema katika eneo hilo
zimetengwa ekari 500 kwa ajili ya EPZA ili kujenga miundombinu
mbalimbali.
“Hilo
eneo ni la uwekezaji kwa ajili ya ujenzi wa viwanda, masoko na maduka
makubwa (malls). Sote tunafahamu kuwa Tanzania hivi sasa inaweka
msisitizo juu ya ujenzi wa viwanda. Pale tunataka tuwe na viwanda vya
nyama, vya kushona nguo na kuchakata madini ya Tanzanite ili kjongeza
thamani,” alisema huku akishangiliwa.
Alisema
kama kuna mtu ana uhakika kuwa nyumba yake bado haijalipwa fidia katika
eneo lile, aende akaonane na Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Joel Bendera lakini
taarifa alizopewa ni kwamba hakuna mtu ambaye hajalipwa.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu amewaita wakurugenzi wa kampuni ya
Tanzanite One ili wampatie taarifa juu ya malalamiko yanayotolewa na
wafanyakazi wa kampuni hiyo kwamba hali ilikuwa nafuu wakati kampuni
hiyo ikimilikiwa na wazungu kuliko hivi sasa.
“Nikimaliza
ziara ya mkoa huu, nataka tarehe 27 Februari, Wakuu wa hii kampuni waje
ofisini kwangu na taarifa kuhusu shughuli za uendeshaji wa madini.
Nitawashirikisha na wabunge wenu ili waje waseme kwa nini mzungu ni bora
kuliko Mtanzania,” alisema.
“Serikali
hii inatarajia kuona Watanzania wakinufaika na rasilmali zao.
Haiwezekani tukahimiza uwekezaji wa ndani halafu leo anasifiwa mzungu
kuliko mzawa,” alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, FEBRUARI 17, 2017.
|
Kuanzia March 1 pombe za VIROBA Marufuku Kuuzwa Hapa Nchini
-
0 comments:
Post a Comment